KARIBU KATIKA KURASA HII UNAOZUNGUMZIA MAISHA YA OSCAR KAMBONA NA UNAWEZA KUTOA MAONI YAKO TAFADHARI USITUMIE LUGHA YA MATUSI AU KUMTUKANA KIONGOZI YOYOTE LENGO LA KURASA HII NI KUKUPA TAARIFA NA MAJARIDIANO KWA USTAARABU KARIBU SANA

Jumapili, 13 Julai 2014

OSCAR KAMBONA NI SHUHUDA WA NYARAKA YA MUUNGANO TANGANYIKA NMA ZANZIBAR



 
  : Kutoka kushoto na ambaye amelekezea uso wake kwenye Camera  ni Marehemu  Oscar Kambona  , Waziri wa mambo ya Nje ya Tanganyika ' na aliyekaa chini akiwa anasaini karatasi ya makubariano ni Rais wa Tanganyika  Julius Nyerere na Makamu wa Rais wa  Zanzibar ' s  Kas Sim Hanga ( Wakishuhudia ) na Rais wa zanzibar  Abeid Karume akitia saini  makubariano ya  Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar  22 April . na ..27 April , 1964 ikawa Jamhuri ya Tanzania 

Jumamosi, 12 Julai 2014

OSCAR KAMBONA NA UKOMBOZI WA BARA LA AFRICA

Marehemu  Oscar Kambona , Waziri wa mambo ya Nje wa Jamhuri ya Zanzibar na Tanganyika kabla haijaitwaa Tanzania  ,Akihutubia jopo la kamati la wakombozi wa Bara la Afrrica Jijini Dar es salaam  hiyo ilikuwa mwaka .8th June 1964

OSCAR KAMBONA AKIHUTUBIA WALINDA AMANI USA.




Waziri wa Mambo ya nje na Ulinzi wa Tanganyika , Oscar S. Kambona, Akizungumza na kikosi cha kujitolea cha walinda Amani  ambapo ilikuwa Tarehe 6 July 1963 ili waje watoe mafunzo kwa jeshi na wananchi wa Tanganyika .Hafla hiyo ilifanyika katika Viwanja vya Bustani ya  Rose Garden, katika Ikulu ya Marekani huko Washington D.C.maarufu kama White House.

Alhamisi, 10 Julai 2014

BBCSWAHILI ILIFUNGULIWA NA MSWAHILI ,OSCAR KAMBONA

Mjane wa Oscar kambona ,Frola akisalimiana na Rais kikwete



 Matangazo ya mwanzo kabisa ya Idhaa ya Kiswahili ya BBC yalitangazwa hewani Juni 27 mwaka wa 1957. Mtangazaji wa kwanza alikuwa marehemu Oscar Kambona ambaye baadae alikuja kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Nje wa Tanganyika na baadaye Tanzania. Katika miaka ya mwanzo mwanzo, matangazo hayo yalikuwa ya dakika 15 peke yake na yalichukuwa nafasi muhimu katika nchi changa zilizokuwa zinainukia katika Afrika Mashariki.
Marais wapigania uhuru
Marais wa kwanza wa Tanzania na Kenya, marehemu Mzee Jomo Kenyatta na Mwalimu Julius Nyerere, mara kwa mara walikuwa wageni mashuhuri kwenye vipindi vya habari wakati walipokuwa wakipigania uhuru wa nchi zao.

Habari na Matukio
Tangu wakati huo Idhaa hii imeendelea kuwahoji viongozi mashuhuri wa kisiasa katika sehemu hiyo, pamoja na kuripoti habari na matukio muhimu Afrika Mashariki na Kati na duniani kote. Matangazo yote yamekuwa yakipeperushwa kutoka London na wakati mwingine huwa tunaungana na studio zetu za Nairobi.

Taarifa sahihi
Kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40 sasa Idhaa yetu imekuwa ikijipatia sifa kemkem kwa kutangaza habari sahihi na motomoto. Kwa mfano Idhaa hii ilikuwa ya kwanza kutangaza taarifa za mauaji ya Dr. Robert Ouko katika mwaka 1990, pamoja na ajali ya ndege iliyowaua Rais Juvenile Habyarimana wa Rwanda na Rais Cyprien Ntayamira wa Burundi mnamo mwaka 1994.

Pia tuliweza kutangaza moja kwa moja kutoka Afrika Mashariki wakati wa uchaguzi wa vyama vingi katika nchi hizo. Kwa mfano, huko Kenya (1992 na 1997), Msumbiji (1994, na 1999), Malawi (1994 na 2000), Tanzania (1995 na 2000), Uganda (1996). Vile vile Idhaa hii ilitangaza taarifa za kuugua, kufariki kwa Mwalimu Julius Nyerere katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas hapa London na kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa mwili wa Rais huyo wa kwanza wa Tanzania.

Mahojiano maalum
Mwishoni mwa mwaka 2000, tulikuwa na mahojiano maalumu na marehemu Laurent Desire Kabila, aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa kipindi cha miaka minne. Haya yalikuwa mazungumzo ya mwisho kabisa aliyoyafanya na mwandishi wa Habari kabla ya kuuawa kwa kupigwa risasi.

Wasikilizaji milioni 10
Kwa sasa Idhaa hii inatangaza kwa muda wa masaa mawili na robo kwa siku, (ikiwa ni pamoja na matangazo kwa. Wasikilizaji wetu wa Afrika ya Kati) au masaa kumi na tano kwa wiki kutoka studio zetu za Bush House, London na Nairobi. Matangazo yetu yanawafikia zaidi ya zaidi ya wasikilizaji milioni kumi kwa wiki.

Jumatano, 9 Julai 2014

HISTORIA YA OSCAR KAMBONA

 
Marehemu Oscar Kambona alizaliwa mwaka 1925 katika kijiji cha Kwambe kilichopo mwambao mwa ziwa Nyasa, karibu na Mbamba-bay, wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma. Alikuwa mtoto wa marehemu Rev. David Kambona na Bibi Miriam Kambona. Rev. Kambona alikuwa ni miongoni mwa waafrika wa kwanza kupata upadre katika kanisa la Anglikana la Tanganyika. 
 Wakati Oscar Kambona akiwa mdogo, baba yake alikuwa akimweleza kuhusu ndoto zake juu ya uhuru wa nchi yake, hivyo Oscar alikuwa akiwa na hamu sana ya kuitumikia nchi yake.
 Oscar alipata elimu ya msingi nyumbani kwao, chini ya mwembe (ambao bado upo), katika kijiji chao kwa kuwatumia wazazi wake wote wawili na mjomba wake, ambao wote walikuwa walimu. Baada ya hapo alipelekwa shule ya kati ya Mt. Barnabas, Liuli, na baadaye shule ya Sekondari ya Alliance, ambako alilipiwa ada na Askofu mzungu wa Anglikana kwa vile baba yake hakuweza kumudu kulipa ada ya paundi 30 kwa mwaka. Oscar alikuwa akisimulia jinsi alivyoweza kumshawishi Askofu huyo amlipie ada kwa kusema sala ya Baba yetu kwa kizungu. Oscar alichaguliwa kwenda ‘Tabora Boy’s Senior Government School’, ambako alionana na Julius Nyerere kwa mara ya kwanza; wakati huo Nyerere alikuwa anafundisha katika shule ya kikatoliki. Baada ya kumaliza masomo ya sekondari alienda katika shule yake iliyopita ya Alliance kama mwalimu na baadae alichaguliwa kuwa ‘Schoolmaster’.
 Ilikuwa katika mkutano wa kitaifa wa walimu, mnamo mwaka 1954, ambapo Kambona na Nyerere walikutana tena. Kambona alikuwa tayari kukitumikia chama cha TANU ambacho kilikuwa kimeanzishwa muda si mrefu, lakini Nyerere akasema wasingeweza kumwajiri kwa vile chama kilikuwa hakina fedha. Kambona akasema chama hakikuwa na fedha kwa vile hakikuwa na ‘organising secretary, na ndipo alipoamua kufanya kazi hiyo ili kujenga chama, bila ya malipo’. Aliishi kwa kutegemea akiba aliyojitunzia kwa kufanya kazi miezi 6. Katika kipindi hiki Kambona alisafiri sehemu mbalimbali za nchi na kuonana na machifu na wazee wa vijiji ili kusajili wanachama. Katika miezi 6 alifanikiwa kusajili wanachama 10,000, na hadi kufikia mwaka mmoja alikuwa amepata wanachama hai 100,000. Kambona alitumia michango aliyopata kufungua akaunti ya kwanza ya TANU. Kisha alienda Butiama kumshawishi Nyerere achukuwe uongozi wa chama moja kwa moja. Baada ya miaka mitatu Kambona aliamua kwenda kusomea sheria katika Chuo cha Middle Temple, nchini Uingereza mwaka 1957 kwa ufadhili wa Gavana. Akiwa London Kambona alikuwa kiongozi wa chama cha wanafunzi wa Tanganyika na Mwenyekiti wa tawi la TANU la London. Ni wakati huo ambapo Kambona alipata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na watu mashuhuri kama George Padmore, mwanaharakati wa umoja wa Afrika, ambaye alimshawishi ahudhurie mkutano wa mwaka 1958 wa waafrika wote(All Africa’s Peoples Conference), uliofanyika nchini Ghana muda mfupi baada ya kupata Uhuru. Akiwa Ghana Kambona alipata nafasi ya kukutana na mwanaharakati mwingine maarufu wa siasa za Afrikla, Kwame Nkurumah. Akiwa uingereza Kambona alikuwa mwaafrika wa kwanza kutangaza taarifa ya habari kwa Kiswahili katika idhaa ya kiswahili ya BBC. Aliporudi nchini Tanganyika, mwaka 1959, TANU ilikuwa imeshaweka bayana madai yake ya kupewa serikali ya madaraka, vinginevyo TANU ilikuwa tayari kuanzisha mapambano kama ilivyokuwa kwa Mau Mau ya Kenya. Wakiwa London wakisubiri kupewa madaraka ya ndani, Nyerere na Kambona walijadili hatua mbalimbali ambazo zingechukuliwa ili kuepuka kutoweka kwa amani. Wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Londoni 1991, Kambona alikumbuka matukio kama hivi, ‘’Bwana Nyerere alikuwa akiishi nami katika chumba kidogo nilichopewa chuoni. Tulijadiliana ni namna gani angeweza kurudi nyumani na kuonana na wafuasi wake bila kupewa serikali ya madaraka. Baadae nilifanikiwa kumshauri kuwa wakati atapozungumza na vyombo vya habari katika the East African Arch aseme kuwa walowezi wa kizungu ambao wapo Tanganyika wana hekima zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki. Alikubali kusema hivyo endapo na yeye Kambona angekubali kukatisha masomo yake ya sheria huko London na kurudi Tanganyika ili ampe nguvu na kumuunga mkono katika kikao cha kamati kuu ya TANU wakati akitetea tamko lake la wenye hekima zaidi. Katika uchaguzi wa kwanza TANU ilishinda viti vyote isipokuwa kimoja. TANU iliunda serikali ya mambo ya ndani chini ya Nyerere ambaye alikuwa Waziri kiongozi wa kwanza. Na katika harakati hizo za matayarisho ya serikali ya ndani, Kambona alimwoa Flora Moriyo wakati wakiwa kwenye msafara wa harakati za kukamilisha matayarisho ya uhuru na serikali ya Uingereza. Harusi ilifungwa katika kanisa la Mt. Paul, London, na Nyerere ndiye alikuwa msimamizi. Kambona aliteuliwa kuwa waziri wa Elimu. Baadaye alishika nyadhifa za waziri wa Mambo ya Ndani, Mambo ya nchi za nje na Ulinzi na Tawala za Mikoa. Pia alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika na mwenyekiti wa utayarishaji wa AOU charter. Mwaka 1964, Kambona alifanya kazi kubwa katika kuunganisha Zanzibar na Tanganyika, akiwa pamoja na Raisi Nyerere, Raisi Karume na Waziri Kiongizi Hanga. Hii ilikuwa ni baada ya mapinduzi ya Zanzibar. Wakati wa wanajeshi wa kikosi cha Calito walipoasi mwaka 1964 Kambona alikuwa msuluhishi mkuu kati ya serikali na wanajeshi hao. Nyerere na Kawawa walienda mafichoni Kigamboni. Baada ya siku tatu za majadiliano Kambona aliafiki kuongeza kasi ya kuwawezesha waafrika kushika hatamu jeshini. Katika mahojiano na gazeti la Daily Telegraph la London Kambona alisema, ‘baada ya kuwatuliza wanajeshi nilikwenda kuwatafuta viongozi wengine na kuwarudisha mjini kwa kutumia Land Rover yangu’. Hatimaye maasi hayo yalidhibitiwa kabisa na majeshi ya Uingereza na Nyerere alimsifu Kambona bushara na uaminifu wake. 
Tofauti kati ya Nyerere na Kambona zilianza kujitokeza baada ya maasi ya wanajeshi. Nyerere alitaka kuanzisha mfumo wa chama kimoja nchini ili kuimarisha usalama. Kambona alipinga hoja hiyo kwa maelezo kwamba mfumo huo ungezorotesha uhuru wa watu na maendeleo ya demokrasia. Hata hivyo, Kambona alishindwa bungeni; alikataa kusaini muswada (bill). Mwaka 1967, baada ya safari ya China ya mwaka 1965, Nyerere akiwa amependezwa na mfumo wa kikomonist wa Mao, alitaka kuanzisha mfumo kama huo kwa jina la ujamaa. Dhana ya msingi ya mfumo wa ujamaa ilikuwa ni kuwahamishia watu katika vijiji vya ujamaa na kutaifisha viwanda ana mali. Kambona hakukubaliana na utaratibu huo kwa maelezo kwamba ungeongeza umaskini na udhibiti wa serikali kwa watu. Alijiuzulu kutoka katika serikali na Chama na hatimaye yeye na familia yake walikimbilia Kenya na kisha Uingereza ambako walipatiwa uhifadhi wa kisiasa. Mara baada ya kuondoka mali za Kambona zilichukuliwa. Ndugu zake wawili, waliwekwa kizuizini bila ya kufikishwa mahakamani na kufungwa kwa zaidi ya miaka kumi. Wanafamilia wengine walinyanyaswa na kuwekwa kizuizini. Wengine kati yao walibambikiziwa kesi za uhaini, wakafikishwa mahakamani na kisha kufungwa na serikali. Kati yao walikuwa Bibi Titi ambaye alipigania uhuru pamoja ana Nyerere na alikuwa kiongozi wa jumuia ya kina mama. Alikuwepo pia Michael Kamaliza ambaye alikuwa mwanaharakati wa chama cha wafanyakazi, mwanachama wa TANU na waziri. 
Wengine ni pamoja na Gray Mattaka, John ana Eliya Chipaka na Prisca Chiombola. Kambona alituhumiwa kuwa kiongozi wa wahaini wakati akiwa London na alihukumiwa bila kuwapo. Watuhumiwa hatimaye walikata rufaa katika mahakama kuu ya Afrika Mashariki na wakaachiwa huru. Hata hivyo, baadae walikamatwa na serikali na kufungwa tena. Kambona alituhumiwa kuwa aliiba pesa nyingi sana zikiwa ni mali ya umma, kitu ambacho Kambona alikataa katika taarifa yake na waandishi wa habari Septemba 6 huko London 1967. Tuhuma hizo zilisema kuwa ‘’ Kambona amekutwa na pesa nyingi sana kama karanga alipopekuliwa katika Uwanja wa ndege Embakasi Nairobi’’ Hata hivyo Kambona katika taarifa yake kwa waandishi wa habari alikanusha kuhusika na tuhuma hizi na badala yake akaipa serikali ya Tanzania kuiomba serikali ya Kenya kutoa ukweli juu ya jambo hilo- jambo halikufanyika. Akiwa Londoni Kambona aliishi maisha ya shida na dhiki. Katika mwaka 1982 ndugu zake Kambona na Otini Kambona walifunguliwa kutoka kizuizini baada ya juhudi za waziri mkuu wa New Zealand Robert Muldoon. Katika mwaka 1990 Kambona akiwa na matumaini makubwa ya mabadiliko ya kisiasa katika Tanzania hususani mabadiliko ya demokrasia, aliunda chama kiitwacho Tanzania Democratic Alliance. 
Wakati vyama vingi vilipoanzishwa Tanzania 1992 Kambona aliomba kurudi Tanzania. Serikali ya Tanzania ilimkatalia katakata na kudai kuwa Kambona hakuwa Mtanzania. Kambona badala yake aliomba Serikali ya Uingereza kumpa pasi ya kusafiria kurudi Tanzania. Hata hivyo Serikali ya Tanzania ilitamka kwamba pamoja na kupata pasi hiyo itamweka ndani pindi atakapoingia Tanzania. Pamoja na msimamo huo wa Serikali, Kambona alitua kwenye ardhi ya Tanzania tarehe 5 september 1992. Hakuna mamlaka iliyomkamata bwana Kambona bali alipewa miezi mitatu awe amekamilisha utata wa uraia wake. 
Baada ya kurudi, Tanzania aliona kuwa harakati za kuelekea kwenye demokrasia ya kweli zilikuwa zikienda kwa mwendo wa kinyonga. Hata hivyo Kambona hakuweza kujihusisha kwa kiasi kikubwa na siasa kutokana na matatizo ya kiafya hususani shinikizo la damu. Hatimaye Oscar Kambona alifariki akiwa katika matibabu mjini London mwezi Juni 1997. Mdogo wake Otini Kambona naye alifariki katika kipindi hichohicho kutokana na magonjwa ya moyo. Wote wawili walizikwa Tanzania, na serikali ya Tanzania iligharimia gharama zote za usafirishaji miili ya marehemu ndugu hawa. Oscar Kambona ameacha mke na watoto wawili. Mtoto wao wa kwanza Mosi Kambona aliuawa mjini London katika mazingira ya kutatanisha. Roho ya Oscar Kambona na ndugu na jamaa wote waliotangulia MWENYEZI MUNGU aziweke pema peponi, Amin.