Marehemu Oscar Kambona alizaliwa mwaka
1925 katika kijiji cha Kwambe kilichopo mwambao mwa ziwa Nyasa, karibu
na Mbamba-bay, wilaya ya Mbinga, Mkoa wa Ruvuma. Alikuwa mtoto wa
marehemu Rev. David Kambona na Bibi Miriam Kambona. Rev. Kambona alikuwa
ni miongoni mwa waafrika wa kwanza kupata upadre katika kanisa la
Anglikana la Tanganyika.
Wakati Oscar Kambona akiwa mdogo, baba yake alikuwa akimweleza kuhusu
ndoto zake juu ya uhuru wa nchi yake, hivyo Oscar alikuwa akiwa na hamu
sana ya kuitumikia nchi yake.
Oscar alipata elimu ya msingi nyumbani
kwao, chini ya mwembe (ambao bado upo), katika kijiji chao kwa kuwatumia
wazazi wake wote wawili na mjomba wake, ambao wote walikuwa walimu.
Baada ya hapo alipelekwa shule ya kati ya Mt. Barnabas, Liuli, na
baadaye shule ya Sekondari ya Alliance, ambako alilipiwa ada na Askofu
mzungu wa Anglikana kwa vile baba yake hakuweza kumudu kulipa ada ya
paundi 30 kwa mwaka. Oscar alikuwa akisimulia jinsi alivyoweza
kumshawishi Askofu huyo amlipie ada kwa kusema sala ya Baba yetu kwa
kizungu.
Oscar alichaguliwa kwenda ‘Tabora Boy’s Senior Government School’,
ambako alionana na Julius Nyerere kwa mara ya kwanza; wakati huo Nyerere
alikuwa anafundisha katika shule ya kikatoliki. Baada ya kumaliza
masomo ya sekondari alienda katika shule yake iliyopita ya Alliance kama
mwalimu na baadae alichaguliwa kuwa ‘Schoolmaster’.
Ilikuwa katika mkutano wa kitaifa wa walimu, mnamo mwaka 1954, ambapo
Kambona na Nyerere walikutana tena. Kambona alikuwa tayari kukitumikia
chama cha TANU ambacho kilikuwa kimeanzishwa muda si mrefu, lakini
Nyerere akasema wasingeweza kumwajiri kwa vile chama kilikuwa hakina
fedha. Kambona akasema chama hakikuwa na fedha kwa vile hakikuwa na
‘organising secretary, na ndipo alipoamua kufanya kazi hiyo ili kujenga
chama, bila ya malipo’. Aliishi kwa kutegemea akiba aliyojitunzia kwa
kufanya kazi miezi 6. Katika kipindi hiki Kambona alisafiri sehemu
mbalimbali za nchi na kuonana na machifu na wazee wa vijiji ili kusajili
wanachama. Katika miezi 6 alifanikiwa kusajili wanachama 10,000, na
hadi kufikia mwaka mmoja alikuwa amepata wanachama hai 100,000. Kambona
alitumia michango aliyopata kufungua akaunti ya kwanza ya TANU. Kisha
alienda Butiama kumshawishi Nyerere achukuwe uongozi wa chama moja kwa
moja.
Baada ya miaka mitatu Kambona aliamua kwenda kusomea sheria katika Chuo
cha Middle Temple, nchini Uingereza mwaka 1957 kwa ufadhili wa Gavana.
Akiwa London Kambona alikuwa kiongozi wa chama cha wanafunzi wa
Tanganyika na Mwenyekiti wa tawi la TANU la London. Ni wakati huo ambapo
Kambona alipata fursa ya kukutana kwa mara ya kwanza na watu mashuhuri
kama George Padmore, mwanaharakati wa umoja wa Afrika, ambaye
alimshawishi ahudhurie mkutano wa mwaka 1958 wa waafrika wote(All
Africa’s Peoples Conference), uliofanyika nchini Ghana muda mfupi baada
ya kupata Uhuru. Akiwa Ghana Kambona alipata nafasi ya kukutana na
mwanaharakati mwingine maarufu wa siasa za Afrikla, Kwame Nkurumah.
Akiwa uingereza Kambona alikuwa mwaafrika wa kwanza kutangaza taarifa ya
habari kwa Kiswahili katika idhaa ya kiswahili ya BBC.
Aliporudi nchini Tanganyika, mwaka 1959, TANU ilikuwa imeshaweka bayana
madai yake ya kupewa serikali ya madaraka, vinginevyo TANU ilikuwa
tayari kuanzisha mapambano kama ilivyokuwa kwa Mau Mau ya Kenya. Wakiwa
London wakisubiri kupewa madaraka ya ndani, Nyerere na Kambona
walijadili hatua mbalimbali ambazo zingechukuliwa ili kuepuka kutoweka
kwa amani.
Wakati akizungumza na waandishi wa habari mjini Londoni 1991, Kambona
alikumbuka matukio kama hivi, ‘’Bwana Nyerere alikuwa akiishi nami
katika
chumba kidogo nilichopewa chuoni. Tulijadiliana ni namna gani angeweza
kurudi
nyumani na kuonana na wafuasi wake bila kupewa serikali ya madaraka.
Baadae
nilifanikiwa kumshauri kuwa wakati atapozungumza na vyombo vya habari
katika
the East African Arch aseme kuwa walowezi wa kizungu ambao wapo
Tanganyika wana hekima zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki. Alikubali
kusema hivyo endapo na yeye Kambona angekubali kukatisha masomo yake ya
sheria huko London na kurudi Tanganyika ili ampe nguvu na kumuunga mkono
katika kikao cha kamati kuu ya TANU wakati akitetea tamko lake la wenye
hekima zaidi.
Katika uchaguzi wa kwanza TANU ilishinda viti vyote isipokuwa kimoja.
TANU
iliunda serikali ya mambo ya ndani chini ya Nyerere ambaye alikuwa
Waziri
kiongozi wa kwanza. Na katika harakati hizo za matayarisho ya serikali
ya ndani,
Kambona alimwoa Flora Moriyo wakati wakiwa kwenye msafara wa harakati za
kukamilisha matayarisho ya uhuru na serikali ya Uingereza. Harusi
ilifungwa
katika kanisa la Mt. Paul, London, na Nyerere ndiye alikuwa msimamizi.
Kambona aliteuliwa kuwa waziri wa Elimu. Baadaye alishika nyadhifa za
waziri
wa Mambo ya Ndani, Mambo ya nchi za nje na Ulinzi na Tawala za Mikoa.
Pia
alikuwa mwenyekiti wa kwanza wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru
za Afrika na mwenyekiti wa utayarishaji wa AOU charter.
Mwaka 1964, Kambona alifanya kazi kubwa katika kuunganisha Zanzibar na
Tanganyika, akiwa pamoja na Raisi Nyerere, Raisi Karume na Waziri
Kiongizi Hanga. Hii ilikuwa ni baada ya mapinduzi ya Zanzibar. Wakati wa
wanajeshi wa kikosi cha Calito walipoasi mwaka 1964 Kambona alikuwa
msuluhishi mkuu kati ya serikali na wanajeshi hao. Nyerere na Kawawa
walienda mafichoni Kigamboni.
Baada ya siku tatu za majadiliano Kambona aliafiki kuongeza kasi ya
kuwawezesha waafrika kushika hatamu jeshini. Katika mahojiano na gazeti
la Daily Telegraph la London Kambona alisema, ‘baada ya kuwatuliza
wanajeshi nilikwenda kuwatafuta viongozi wengine na kuwarudisha mjini
kwa kutumia Land Rover yangu’. Hatimaye maasi hayo yalidhibitiwa kabisa
na majeshi ya Uingereza na Nyerere alimsifu Kambona bushara na uaminifu
wake.
Tofauti kati ya Nyerere na Kambona zilianza kujitokeza baada ya maasi ya
wanajeshi. Nyerere alitaka kuanzisha mfumo wa chama kimoja nchini ili
kuimarisha usalama. Kambona alipinga hoja hiyo kwa maelezo kwamba mfumo
huo ungezorotesha uhuru wa watu na maendeleo ya demokrasia. Hata hivyo,
Kambona alishindwa bungeni; alikataa kusaini muswada (bill).
Mwaka 1967, baada ya safari ya China ya mwaka 1965, Nyerere akiwa
amependezwa na mfumo wa kikomonist wa Mao, alitaka kuanzisha mfumo kama
huo kwa jina la ujamaa. Dhana ya msingi ya mfumo wa ujamaa ilikuwa ni
kuwahamishia watu katika vijiji vya ujamaa na kutaifisha viwanda ana
mali. Kambona hakukubaliana na utaratibu huo kwa maelezo kwamba
ungeongeza umaskini na udhibiti wa serikali kwa watu. Alijiuzulu kutoka
katika serikali na Chama na hatimaye yeye na familia yake walikimbilia
Kenya na kisha Uingereza ambako walipatiwa uhifadhi wa kisiasa.
Mara baada ya kuondoka mali za Kambona zilichukuliwa. Ndugu zake wawili,
waliwekwa kizuizini bila ya kufikishwa mahakamani na kufungwa kwa
zaidi ya miaka kumi. Wanafamilia wengine walinyanyaswa na kuwekwa
kizuizini. Wengine kati yao walibambikiziwa kesi za uhaini, wakafikishwa
mahakamani na kisha kufungwa na serikali. Kati yao walikuwa Bibi Titi
ambaye alipigania uhuru pamoja ana Nyerere na alikuwa kiongozi wa jumuia
ya kina mama. Alikuwepo pia Michael Kamaliza ambaye alikuwa
mwanaharakati wa chama cha wafanyakazi, mwanachama wa TANU na waziri.
Wengine ni pamoja na Gray Mattaka, John ana Eliya Chipaka na Prisca
Chiombola. Kambona alituhumiwa kuwa kiongozi wa wahaini wakati akiwa
London na alihukumiwa bila kuwapo. Watuhumiwa hatimaye walikata rufaa
katika mahakama kuu ya Afrika Mashariki na wakaachiwa huru. Hata hivyo,
baadae walikamatwa na serikali na kufungwa tena.
Kambona alituhumiwa kuwa aliiba pesa nyingi sana zikiwa ni mali ya umma,
kitu ambacho Kambona alikataa katika taarifa yake na waandishi wa
habari Septemba 6 huko London 1967. Tuhuma hizo zilisema kuwa ‘’ Kambona
amekutwa na pesa nyingi sana kama karanga alipopekuliwa katika Uwanja
wa ndege Embakasi Nairobi’’ Hata hivyo Kambona katika taarifa yake kwa
waandishi wa habari alikanusha kuhusika na tuhuma hizi na badala yake
akaipa serikali ya Tanzania kuiomba serikali ya Kenya kutoa ukweli juu
ya jambo hilo- jambo halikufanyika.
Akiwa Londoni Kambona aliishi maisha ya shida na dhiki. Katika mwaka
1982 ndugu zake Kambona na Otini Kambona walifunguliwa kutoka kizuizini
baada ya juhudi za waziri mkuu wa New Zealand Robert Muldoon.
Katika mwaka 1990 Kambona akiwa na matumaini makubwa ya mabadiliko ya
kisiasa katika Tanzania hususani mabadiliko ya demokrasia, aliunda chama
kiitwacho Tanzania Democratic Alliance.
Wakati vyama vingi
vilipoanzishwa Tanzania 1992 Kambona aliomba kurudi Tanzania. Serikali
ya Tanzania ilimkatalia katakata na kudai kuwa Kambona hakuwa Mtanzania.
Kambona badala yake aliomba Serikali ya Uingereza kumpa pasi ya
kusafiria kurudi Tanzania. Hata hivyo Serikali ya Tanzania ilitamka
kwamba pamoja na kupata pasi hiyo itamweka ndani pindi atakapoingia
Tanzania. Pamoja na msimamo huo wa Serikali, Kambona alitua kwenye ardhi
ya Tanzania tarehe 5 september 1992. Hakuna mamlaka iliyomkamata bwana
Kambona bali alipewa miezi mitatu awe amekamilisha utata wa uraia wake.
Baada ya kurudi, Tanzania aliona kuwa harakati za kuelekea kwenye
demokrasia ya kweli zilikuwa zikienda kwa mwendo wa kinyonga. Hata hivyo
Kambona hakuweza kujihusisha kwa kiasi kikubwa na siasa kutokana na
matatizo ya kiafya hususani shinikizo la damu. Hatimaye Oscar Kambona
alifariki akiwa katika matibabu mjini London mwezi Juni 1997. Mdogo wake
Otini Kambona naye alifariki katika kipindi hichohicho kutokana na
magonjwa ya moyo. Wote wawili walizikwa Tanzania, na serikali ya
Tanzania iligharimia gharama zote za usafirishaji miili ya marehemu
ndugu hawa.
Oscar Kambona ameacha mke na watoto wawili. Mtoto wao wa kwanza Mosi
Kambona aliuawa mjini London katika mazingira ya kutatanisha.
Roho ya Oscar Kambona na ndugu na jamaa wote waliotangulia MWENYEZI
MUNGU aziweke pema peponi, Amin.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni